Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Samuel Sitta alisema
jana kwamba kutokana na kutokea kwa mivutano baina ya wadau wa usafiri
nchini mara kwa mara na kusababisha usumbufu kwa wananchi, Jumamosi
iliyopita, Waziri Pinda aliunda tume itakayokuwa ikishughulikia matatizo
yanayojitokeza.
“Lengo la kamati hii ni kuhakikisha kwamba wakati
wote bila kusubiri migomo, kuwe na majadiliano shirikishi ya wadau wote
ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya makundi mbalimbali katika usafiri wa
barabarani,” alisema Sitta.
Aliwataja wanaounda kamati hiyo kuwa ni Katibu
Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, ambaye atakuwa mwenyekiti na katibu wake
atakuwa Kamishna wa Polisi, Usalama Barabarani.
Wajumbe ni katibu mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani
(Usimamizi wa Polisi na usalama barabarani) na katibu mkuu, Wizara ya
Kazi na Ajira (Mikataba ya ajira kati ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi
Tanzania (Taboa)/Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) na
madereva).
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Masuala
ya sheria), naibu katibu mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, mkuu wa uratibu na
Idara ya Maafa, mwenyekiti Taboa, mwenyekiti wa Tatoa
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi na
Magari ya Mizigo, mwenyekiti wa chombo cha kusimamia haki za wasafiri na
mkurugenzi wa Sumatra.
Kamati hiyo imetangazwa siku ambayo huduma za usafiri wa barabara zilisimama kutokana na mgomo wa madereva.
Mbagala mshikemshike
Mabomu ya machozi yaliyotupwa na polisi yalikuwa
salama wananchi wenye magari binafsi baada ya kuwatimua mamia ya vijana
waliokuwa wamefunga Barabara ya Kilwa eneo la Zakhiem na kusababisha
msongamano mkubwa wa magari.
Vijana hao walifunga barabara na kuanza kushusha
abiria kwenye magari binafsi na kuwalazimisha wenye magari hayo
kuwapakia wanafunzi na kuwapeleka shule.
Shughuli hiyo hilo lililodumu kwa dakika 40
kuanzia saa 1.45 hadi saa 2.25 asubuhi. Vijana nao waliwashusha
wafanyakazi wote waliokuwa kwenye basi la Kampuni ya Tanzania Road
Haulage (TRH) waliokuwa wakienda kazini na kumlazimisha dereva kuwapakia
wanafunzi na kuwapeleka shule.